Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA SHEREHE ZA MIAKA 53 YA MUUNGANO UWANJA WA JAMHURI, DODOMA, 26 APRILI, 2017

Wednesday 26th April 2017

Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa     Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;

 

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

 

Mheshimiwa Kassim Majaliwa,

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar;

 

Mheshimiwa Job Ndugai,

         Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza          la Wawakilishi;

 

MheshimiwaProf. Ibrahim Juma, Kaimu Jaji Mkuu         wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;

 

Waheshimiwa Mzee Mwinyi na Mzee Kikwete, Marais Wastaafu wa Awamu ya Pili na Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Dkt. Gharib Bilal,

Makamu wa Rais Mstaafu wa Tanzania;

 

Waheshimiwa Mawaziri Wakuu Wastaafu wa       Tanzania mliopo;

 

Waheshimiwa Wake wa Viongozi Wakuu      Wastaafu, mkiongozwa na Mama Maria Nyerere na Mama Fatuma Karume;

 

Waheshimiwa Mawaziri mliopo;

 

Mheshimiwa Balozi John Kijazi, Katibu Mkuu       Kiongozi;

 

Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;

 

Mheshimiwa Jordan Rugimbana, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;

 

Waheshimiwa Wabunge;

 

Waheshimiwa Mabalozi na Viongozi wa Taasisi za       Kimataifa;

 

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa na   Dini mliopo;

 

Wageni waalikwa wote;

 

Wananchi Wenzangu, Mabibi na Mabwana:

 

Kwanza kabisa, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kuiona siku hii ya leo. Tunamshukuru pia kwa kuendelea kulilea taifa letu na kulifikisha salama hapa tulipo.

 

Aidha, napenda nitumie fursa hii kutuma salamu nyingi za pongezi kwa Watanzania wote kwa kuadhimisha Miaka hii 53 ya Muungano wetu na kuzaliwa taifa letu. Hakuna shaka, hii ni siku muhimu na ya kihistoria kwa taifa letu. Hivyo, kila Mtanzania, mahali popote alipo, hana budi kuifurahia na kujivunia.Hii ndio sherehe ya Birthday ya nchi yetu.

Ndugu wananchi, Mabibi na Mabwana:

Kama mnavyofahamu, siku kama ya leo Mwaka 1964 taifa jipya, la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilizaliwa. Taifa hili jipya lilizaliwa baada ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kutia saini Hati ya Muungano kuunganisha nchi hizi mbili na kuunda taifa moja.

 

Yapo mambo mengi yaliyowezesha kwa Muungano wetu. Jambo la kwanza ni niudugu wa kihistoria uliokuwepo baina ya wananchi wa mataifa yetu mawili. Kabla hata ya kuja kwa wakoloni, wananchi wa mataifa haya mawili walikuwa wakishirikiana kwenye masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Kutokana naushirikiano huo, baadhi ya Watanganyika walilowea Zanzibar na walikuwepo Wazanzibari waliolowea Tanganyika. Hapana shaka, hii ndio sababu leo tunao akina Jaji Makungu. Uhusiano huu wa kidugu ndio ulirahisha mataifa yetu kuungana mara tu baada ya kupata uhuru wao.

 

Sababu ya pili iliyosababisha kuanzishwa kwa Muungano wetu ni uhusiano na ushirikiano mzuri uliokuwepo kati ya vyama vyetu vya ukombozi, kwanza kabisa wakati wa Tanganyika African Association (TAA) na African Association na baadaye TANU na ASP. Viongozi na wanachama wa vyama hivi viwili walikuwa na ushirikiano wa karibu.  Walikuwa wanatembeleana, kubadilishana mawazo na kusaidiana kwa hali na mali. Hivyo, kutokana na uhusiano na ushirikiano mzuri uliokuwepo kati ya vyama hivi viwili, haikuwa jambo gumu kuunganisha mataifa haya mawili baada ya uhuru.

 

Ndugu Watanzania wenzangu, Mabibi na Mabwana;

Leo tunaposheherekea Sikukuu ya Muungano, sisi Watanzania ni lazima tutafakari mustakabali wa Taifa letu. Kama mnavyofahamu, wengi wa Watanzania wa sasa wamezaliwa baada ya Muungano. Tutumie basi sherehe hizi katika kutafakari mahali tulikotoka, mahali tulipo na kule tunakoelekea. Ni kwa namna hiyo tu tutaweza kuulinda na kuudumisha Muungano wetu.

 

 Katika kipindi cha Miaka 53 ya Muungano wetu, nchi yetu imefanikiwa kupata mafanikio makubwasana. Nitataja makubwa matatu.Mosi, kwa kuunganisha Mataifa yetu mawili tumeweza kuunda Taifa moja lenye nguvu. Hii imetuwezesha kulinda uhuru amani na umoja wetu. Nchi yetu imebaki kuwa na amani na mipaka yetu ipo salama. Na tunajiamulia mambo yetu sisi wenyewe.

 

Pili, Muungano wetu umetuwezesha kupata mafanikio makubwa katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii. Serikali zetu mbili, yaani Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar, zimefanya jitihada kubwa za kukuza uchumi na kukabiliana na matatizo ya umaskini na ukosefu wa ajira. Tumejenga miundombinu ya usafiri wa anga, majini, reli na nchi kavu. Miradi ya umeme pia imejengwa.Aidha, tumeimarisha na kuboresha upatikanaji wa huduma za jamii. Idadi ya shule na hospitali zimeongezeka. Upatikanaji wa huduma za maji nazo zimeimarika. Demokrasia  imepanuka. Kwa ujumla, naweza kusema kuwa Tanzania ya sasa sio ile ya mwaka 1964.

 

Tatu, nchi yetu inaheshimika kimataifa na inatoa mchango mkubwa katika ngazi ya Kanda, Bara na duniani kwa ujumla. Tumeshiriki katika harakati za ukombozi wa Bara letu na tunaendelea kushiriki kwenye shughuli za kutafuta amani sehemu mbalimbali duniani. Haya ni baadhi tu ya mafanikio. Yapo mengine mengi.

 

Ndugu Watanzania wenzangu, Mabibi na Mabwana:

Wahenga husema “usione vyaelea, vimeundwa”. Mafanikio niliyoyataja hayakujileta. Wapo watu ambao wamefanya kazi mchana na usiku kuhakikisha yanapatikana. Kama mnavyofahamu, kulinda Muungano kama wetu sio jambo rahisi. Yapo mataifa mengi yaliyojaribu lakini yameshindwa. Lakini wengi wetu hapa pia tunafahamu kuwa hata  kulinda muungano wa ndoa kati ya watu wawili sio jambo rahisi. Hivyo basi, hatuna budi kuwapongeza wote waliowezesha nchi yetu kufikisha Miaka hii 53 ya Muungano.

 

Nafahamu wapo watu wengi waliotoa mchango wao, lakini kwa leo nitawataja wachache. Kwanza kabisa, napenda kwa niaba yenu, niwashukuru na kuwapongeza sana viongozi wetu wakuu waasisi, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Kwanza wa Tanganyika na Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar kwa kuwezesha Muungano huu. Kama nilivyosema, hawa ndio waasisi wa Muungano huu. Hawa ndio walisaini Hati za Muungano. Tunawashukuru sana Waasisi wetu hawa wawili; Bahati nzuri leo hapa tunao wajane wa waasisi hao, Mama Maria Nyerere na Mama Fatuma Karume ambao wamekuja kuungana nasi katika kusheherekea siku hii muhimu kwa taifa letu.

 

Sambamba nao, nawapongeza viongozi wetu waliowafuatia, wa awamu zote za Serikali zetu mbili, kwa uongozi wao bora uliowezesha Muungano wetu kudumu, kustawi na kuzidi kuimarika mpaka sasa.  Nimefarijika sana kuwaona Marais Wastaafu Mzee Mwinyi na Mzee Kikwete; Mawaziri Wakuu Wastaafu, na viongozi wengine wastaafu tuko nao hapa. Wote kwa pamoja, tunawashukuru sana. Napenda kutumia fursa hii kuahidi kuwa mimi pamoja na mwezangu, Mheshimiwa Rais Dkt. Shein, tutafuata nyayo za viongozi waliotutangulia katika kuulinda na kuudumisha Muungano wetu.

 

 

 

Ndugu Watanzania wenzangu, Mabibi na Mabwana:

Licha ya mafanikio ya Muungano tuliyoyapata,ni dhahiri kuwa bado zipo changamoto. Lakini kwa bahati nzuri tunayo Kamati ya Pamoja inayoshughulikia masuala ya Muungano, ambayo Mwenyekiti wake ni Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu. Wajumbe wengine ni pamoja na Waziri Mkuu, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Serikali zote mbili. Kamati hii inafanya kazi nzuri sana, hata hivyo, hatupaswi kuiachia Kamati ifanye mambo yote. Ni lazima kila Mtanzania mahali popote alipo ahakikishe anafanya jitihada za kuuimarisha na kuulinda Muungano wetu.

 

Ni kwa sababu hii nimefurahishwa sana na kaulimbiu ya Sherehe za Muungano mwaka huu ambayo inasema “Miaka 53 ya Muungano: Tuulinde na Kuuimarisha, Tupige Vita Madawa ya Kulevya na Kufanya Kazi kwa Bidii”. Kaulimbiu hii ni muafaka na imekuja kwa wakati. Kila Mtanzania anao wajibu wa kulinda Muungano wetu. Na njia bora ya kuulinda na kuuimarisha Muugano wetu ni kuchapa kazi kwa bidii.

 

Waheshimiwa Viongozi na Wageni Waalikwa;

 Ndugu Watanzania wenzangu, Mabibi na Mabwana:

Kabla sijahitimisha hotuba yangu hii fupi, ninayo masuala mawili ningependa kugusia. Mosi, hii nimara ya kwanza katika historia ya Muungano wetu, Maadhimisho ya Muungano yanafanyika hapa Dodoma, Makao Makuu ya nchi yetu. Hii ni ishara tosha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Chama Cha Mapinduziimedhamiria kwa dhati kabisa kuhamishia Makao Makuu ya Serikali hapa Dodoma. Na niwahakikishie wana-Dodoma na Watanzania kwa ujumla kuwa, kama tulivyoahidi, ifikapo mwaka 2020, Serikali yote itakuwa imehamia Dodoma.

 

Bahati nzuri, hatua za kuhamia Dodoma tayari zimeanza. Viongozi Wakuu wa Wizara zote, yaani Mawaziri, Naibu Mawaziri; Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na baadhi ya Wakurugenzi na watumishi wameshahamia hapa Dodoma. Zaidi ya watumishi 3,000 nao wameshahamia. Awamu ya Pili na Tatu ya kuhamia Dodoma imepangwa kutekelezwa mwaka ujao wa fedha, ambapo Serikali imetenga takriban shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kujenga ofisi na nyumba za viongozi wa Serikali. Natumaini Bunge litapitisha Bajeti hiyo. Sambamba na hilo, tunaendelea na jitihada za kujenga miundombinu ya usafiri ya kuja na kutoka hapa Dodoma. Tumeshapanua uwanja wa ndege (na tutaendelea kuupanua) na hivi majuzi nimeweka Jiwe la Msingi la kuanza ujenzi wa Reli ya Kati ya kisasa ambayo itapita hapa Dodoma. Tunaendelea na ujenzi wa barabara mbalimbali na tuna mipango kabambe ya kuboresha upatikanaji wa umeme na maji pamoja na huduma za afya na elimu. Maandalizi ya ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Kisasa kwa ufadhili wa Serikali ya Morocco yanaendelea vizuri.

 

Tunachukua hatua hizi zote kuufanya mji huu wa Dodoma ukidhi mahitaji ya kuwa Makao Makuu ya Serikali. Hivyo basi, niwaombe wakazi wa Dodoma pamoja na Mikoa jirani ya Singida, Arusha, Iringa na Morogoro kujipanga vizuri kutumia fursa zitakazotokana na uamuzi wa kuhamishia Makao Makuu hapa Dodoma.

 

Jambo la pili ambalo ningependa kulizungumzia ni kuhusu umuhimu wa kudumisha amani yetu. Tumeweza kufikisha miaka 53 ya Muungano kwa sababu ya kuwepo kwa amani. Na tumeweza kupata mafanikio yote niliyoyataja kwa sababu ya uwepo wa amani hapa nchini. Bila ya amani, mambo yote haya yasingewezekana. Hivyo basi, kila Mtanzania ni lazima ashiriki katika kulinda na kudumisha amani yetu.

Waheshimiwa Viongozi na Wageni Waalikwa;

 Ndugu Watanzania wenzangu, Mabibi na Mabwana:

Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kutoa shukrani kwa Kamati ya Maandalizi kwa kufanikisha Maadhimisho haya. Maadhimisho yamefana. Uwanja umefurika na bado nje kuna watu wengi . Hongereni sana wana-Kamati.

 

Napenda pia kuwashukuru wageni wetu waalikwa waliokuja hapa kushiriki nasi katika shughuli hii muhimu na kihistoria kwa taifa letu.Tunawashukuru Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi mbalimbali za Kimataifa.

 

Tunavishukuru vyombo vya ulinzi na usalama, vikundi vya burudani, chipukizi na waandishi wa habari kwa kufanikisha sherehe hii. Napenda pia kutoa shukrani nyingi kwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma, chini wa kiongozi wenu Mheshimiwa Rugimbana, kwa kutukaribisha vizuri kwenye Mkoa wenu. Mmedhihirisha kuwa hapa kweli ni Makao Makuu ya Nchi yetu.

Ndugu Watanzania wenzangu, Muungano wetu ndio umoja wetu; ndio nguvu yetu na silaha yetu. Hivyo basi, hatuna budi kuulinda na kuudumisha. Kwa sababu hiyo, napenda kurudia tena kuwa mimi na mwenzangu, Mheshimiwa Rais Shein, tutaulinda kwa nguvu zetu zote. Yeyote atakayejaribu kuuvunja Muungano wetu, atatangulia kuvunjika yeye kwanza.

 

Mungu Ibariki Tanzania!

Mungu Wabariki Watanzania!

“Ahsanteni Sana kwa kunisikiliza