Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE KILELE CHA SIKUKUU YA WAFANYAKAZI DUNIANI MOSHI, KILIMANJARO, TAREHE 1 MEI, 2017

Monday 1st May 2017

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais

wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu

wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Bunge

la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Tulia Ackson, Naibu Spika

wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; 

 

Ndugu Tumaini Nyamhokya, Rais wa Shirikisho

la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania;

 

Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,

Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu;

 

Waheshimiwa Mawaziri mliopo;

 

Mheshimiwa Bolozi John Kijazi, Katibu Kiongozi;

 

Waheshimiwa Makatibu Wakuu mliopo;

 

Mheshimiwa Mecky Sadick, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro;

 

Mheshimiwa Mary Kawar, Mkurugenzi wa Shirika         la Kazi Duniani,

Ofisi za Afrika Mashariki;

Waheshimiwa Majaji mliopo;

 

Mheshimiwa Almas Maige, Mwenyekiti

Chama cha Waajiri Tanzania;

 

Waheshimiwa Wabunge mkiongozwa na Mbunge wa Moshi Mjini;

 

 Waheshimiwa Mabalozi mliopo;

 

Mheshimiwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi;

 

Ndugu Reginald Mengi, Mwenyekiti wa Sekta Binafsi Tanzania;

 

Ndugu Dkt. Yahya Msigwa, Katibu Mkuu wa         Shirikisho

la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA);

 

Ndugu Dkt. Aggrey Mlimuka, Mkurugenzi Mtendaji

wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE);

 

Viongozi wa Serikali, Vyama vya Siasa na Dini mliopo;

 

Ndugu Wafanyakazi Wenzangu;

 

Wanahabari, Mabibi na Mabwana:

 

         Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na kutuwezesha kukutana hapa tukiwa salama. Aidha, napenda na mimi nikiri kuwa sijawahi kuona kwenye sherehe za Mei Mosi umati mkubwa kama huu. Hii inanipa shida hata mimi ya namna ya kujibu hoja nilizoelezwa na Katibu Mkuu wa TUCTA. Lakini kwa ujumla, niseme tu kwamba leo Moshi mmevunja rekodi na kwa kweli mmenipa nguvu kubwa sana ya kuwatumikia. Na namwomba Mwenyezi Mungu anisaidie ili nisiwaangushe katika kuwatumikia.

 

         Napenda pia kutumia fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa Uongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), wakiongozwa na Rais wa Shirikisho, Ndugu Tumaini Nyamhokya kwa kunialika kuwa Mgeni Rasmi katika Siku hii muhimu kwa Wafanyakazi Duniani. Aidha, nawapongeza Viongozi Wapya wa TUCTA kwa kuchaguliwa kwenu kuongoza Shirikisho hili. Hakuna shaka, ushindi mlioupata ni kielelezo cha imani kubwa waliyonayo Wafanyakazi wa Tanzania juu yenu. Nawatakia utekelezaji mwema wa majukumu yenu mpya. Na kwa namna ambavyo mmeanza nina ukakika kabisa mtayamudu vyema.

 

Binafsi,nimeshakutana nanyi mara moja pale Ikulu, Dar es Salaam, ambapo tulifanya mazungumzo. Kwa kile ambacho nilikiona katika mazungumzo yetu, ni dhahiri kuwa mmedhamiria kwa dhati kuwasaidia wafanyakazi na nchi yetu kwa ujumla. Napenda kurudia ahadi niliyotoa siku ile kwamba,mimi pamoja na wenzangu Serikalini, tutawapa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yenu.

 

Ndugu Wafanyakazi Wenzangu, Mabibi na Mabwana;

         Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru wana-Kilimanjaro kwa kukubali kuwa wenyeji wa maadhimisho haya. Tunawashukuru pia kwa mapokezi makubwa na kwa ukarimu mliotuonesha tangu tumewasili. Lakini kwa kuwa hii ni mara yangu ya kwanza kufika katika Mkoa wa Kilimanjaro tangu nimechaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda niwashukuru wana-Kilimanjaro kwa maombezi na kura zenu zilizoniwezesha kuchaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Nchi yetu. Ahsanteni sana.

 

         Uchaguzi sasa umekwisha, jukumu kubwa ambalo lipo mbele yetu kwa sasa ni kujenga Taifa letu. Mimi ni Rais wa Watanzania wote. Nitafanya kazi kwa maslahi ya Watanzania wote. Na napenda niwaahidi wana-Kilimanjaro kuwa yale yote tuliyoahidi wakati wa kampeni tutayatekeleza. Na kwa kweli, tayari mambo mengi tumeshaanza kutekeleza, ambayo sina shaka mengi mnayafahamu.

 

Tumeongeza wastani wa ukusanyaji wa mapato kwa mwezi kutoka shilingi bilioni 850 hadi kufikia shilingi trilioni 1.3, na tumeweza kubana matumizi yasiyo ya msingi. Hii imetuwezesha kuongeza bajeti ya maendeleo kutoka wastani wa asilimia 26 za awali hadi kufikia asilimia 40. Tunajenga na kuimarisha miundombinu ya usafiri, umeme na maji. Tumenunua ndege sita mpya, ambazo nina uhakika zitakuza utalii, hususan katika Mkoa huu wa Kilimanjaro. Watalii sasa watakuja hapa moja kwa moja bila kupitia nchi jirani.

 

Tunatoa elimu bila malipo kutoka shule ya msingi hadi sekondari, kama tulivyoahidi, ambapo Serikali inatenga kiasi cha shilingi bilioni 18.77 kila mwezi kugharamia.Tumeongeza idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo ya elimu ya juu kutoka 98,300, wakati tunaingia madarakani, hadi kufikia 124,198, hivi sasa.Tumeongeza bajeti ya kununua madawa kutoka shilingi bilioni 31 hadi kufikia shilingi bilioni 250.

 

Leo sio siku ya kueleza mafanikio ambayo tayari tumepata. Leo ni Siku ya Wafanyakazi. Hivyo basi, itoshe tu kusema kuwa tangu tumeigia madarakani, Serikali imefanya mambo mengi yenye manufaa kwa taifa letu na watu wake, wakiwemo wafanyakazi.

 

Ndugu Wafanyakazi, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

         Hakuna shaka,leo ni siku muhimu. Kama mnavyofahamu, Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani, maarufu kama Mei Mosi; ni siku muhimu sio tu hapa nchini bali duniani kote. Ni siku ambayo wafanyakazi duniani kote wanapata fursa ya kukumbushana kuhusu umuhimu wa kujenga umoja na mshikamano katika kutetea maslahi yao. Ni siku ambayo wafanyakazi wanapata fursa ya kutafakari masuala yanayowahusu, hususan kwa kuanisha changamoto zinazowakabili na kupendekeza mikakati ya kuzishughulikia. Lakini, mbali na hayo, Mei Mosi, ni siku ambayo hutumika Duniani kote kutambua na kuenzi mchango unaotolewa na wafanyakazi katika shughuli za maendeleo.

 

         Kama mnavyofahamu, wafanyakazi ndio injini ya maendeleo ulimwenguni kote. Hakuna jambo la maendeleo limewahi kufanyika hapa duniani ambalo wafanyakazi hawajashiriki. Katika kila jambo, wanahusika. Kuanzia kwenye shughuli za kilimo, uvuvi, ufugaji, utalii, ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi, ulinzi wa amani na usalama, utoaji wa huduma za jamii, maendeleo ya sayansi na teknolojia, n.k. Kote wafanyakazi wanahusika.

 

         Ni kwa sababu hiyo, napenda kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Serikali, kutumia fursa hii kuwapongeza sana Wafanyakazi wote, hususan Wafanyakazi wa Tanzania, kwa kuadhimisha siku hii; na kwa mchango wenu mkubwa katika maendeleo ya taifa letu. Serikali inatambua mchango wenu mkubwa na tunawasihi sana muendelee kujituma na kuchapakazi kwa bidii. Maendeleo ya taifa letu, kwa kiasi kikubwa, yanawategemea ninyi. Serikali itaendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili ili muweze kufanya kazi katika mazingira mazuri.

 

Ndugu Viongozi wa TUCTA na Ndugu Wafanyakazi wenzangu;

         Muda mfupi uliopita tumesikia Risala ambayo imesomwa kwa ufasaha mkubwa na Katibu Mkuu wa TUCTA, Dkt. Msigwa.  Ni Risala ambayo inajieleza yenyewe. Na bahati nzuri, viongozi wote muhimu ambao wanapaswa kushughulikia hoja zilizotolewa na TUCTA wapo hapa. Kuanzia Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika wa Bunge, Naibu Spika, Mawaziri na Katibu Mkuu Kiongozi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wabunge; wote wapo hapa. Hivyo, nina imani wamesikia mambo yaliyoelezwa na watayashughulikia.

 

Na napenda niwahakikishie ndugu wafanyakazi wenzangu kuwa Serikali imesikia na itazifanyia kazi hoja zenu zote. Sisi kwa upande wetu tumedhamiria kwa dhati kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano na Wafanyakazi. Tutaimarisha uhusiano na ushirikiano wetu na Vyama vya Wafanyakazi pamoja Chama cha Waajiri. Tutaujenga na kuimarisha kikamilifu utatu huu. Ombi langu kwenu wafanyakazi endeleeni kuiunga mkono Serikali, hususan kwa kuchapa kazi kwa bidii. 

 

Ndugu Viongozi wa TUCTA na Ndugu Wafanyakazi wenzangu;

Kama nilivyosema, Risala ya Katibu Mkuu wa TUCTA imeeleza hoja nyingi.  Lakini niseme tu kwamba hoja na madai mengi yaliyowasilisha sio mageni. Ni masuala ya muda mrefu. Na baadhi Serikali ilishaanza kushughulikiwa na tumefikia hatua nzuri. Mathalan, katika Risala yenu, mmeomba kuboreshwa kwa mfumo wa Hifadhi ya Jamii, hususan kuanzishwa kwa Fao la Kukosa Ajira, kama mbadala wa Fao la Kujitoa ambalo limefutwa kwa Sheria Na. 5 ya mwaka 2012. Napenda kuwaarifu kuwa Serikali inaendelea na taratibu za kuanzisha Fao la Kujitoa/Bima ya Ajira ili kuwawezesha wafanyakazi ambao ni wanachama wa Mifuko ya Pensheni kulipwa sehemu ya michango yao kwa mujibu wa sheria pindi wanapopoteza ajira kabla ya kufikisha umri wa kustaafu. Utaratibu wa kuanzisha Fao/Bima hiyo unaendelea vizuri. Wadau, wakiwemo waajiri na vyama vya wafanyakazi, wameshatoa maoni yao. Na nimearifiwa kuwa, hivi karibuni, Muswada wa Sheria wa kuanzisha Fao hilo utapelekwa Bungeni. Na Bunge likipitisha, siku hiyo hiyo nitasaini.

 

         Kuhusu Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pia, mmezungumzia suala la kuharakisha kuundwa kwa mifuko miwili ili kupunguza utitiri wa mifuko hiyo na hatimaye kupunguza gharama za uendeshaji. Kama mnavyofahamu, suala hili lilikwishakubaliwa na Serikali na tumefikia hatua nzuri. Wadau muhimu, mkiwemo ninyi vyama vya wafanyakazi pamoja na waajiri, tayari mmetoa maoni na mapendekezo kuhusu namna ya kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii. Kwa sasa Waraka wa Baraza la Mawaziri unaandaliwa ili hatimaye itungwe sheria itakayowezesha kuunganisha mifuko ya hifadhi ili ibaki miwili. Zoezi hili likikamilika, tutakuwa tumepata mwarobaini wa tatizo la tofauti ya fomula ya ukokotoaji wa mafao, ambalo nalo ni moja ya malalamiko ya wafanyakazi nchini.

 

         Risala yenu pia imeeleza kuhusu suala la ucheleweshaji wa malipo ya mafao. Hili nalo Serikali inalishughulikia tena kwa nguvu sana. Kama mnavyofahamu, suala hili la ucheleweshaji, kwa kiwango kikubwa, lilikuwa linasababishwa na waajiri kushindwa au kuchelewa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao. Na mmoja wa waajiri hao ni Serikali. Mathalan, wakati tunaingia madarakani, Serikali ilikuwa inadaiwa takriban shilingi trilioni 1.5 kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. Tangu wakati huo, tumeshalipa shilingi trilioni 1.23. Na zilizobaki tutazilipa hivi karibuni.

 

Kufuatia Serikali kulipa deni hilo, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii sasa inawalipa wastaafu mafao yao kwa wakati. Na hii sasa itaipa nguvu Serikali ya kufuatilia na kuwahimiza waajiri wengine, hususan wa sekta binafsi, kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati.

 

Ndugu Viongozi wa TUCTA na Ndugu Wafanyakazi wenzangu;

         Suala jingine ambalo mmelieleza vizuri kwenye Risala yenu ni kuhusu Usalama Kazini, Afya na Gonjwa la Ukimwi. Haya ni masuala ambayo hayana mjadala. Hivyo, naahidi tutayasimamia na kuyatekeleza.

 

         Kwenye Risala pia limegusiwa suala la Uhuru wa Wafanyakazi Kujiunga na Vyama vyao. Suala hili nilishalizungumzia mwaka jana. Lakini napenda kurudia tena leo. Vyama vya wafanyakazi mahali pa kazi si suala la hiari. Lipo kwa mujibu wa sheria. Hivyo basi, hakuna sekta, kampuni wala mwekezaji aliye juu ya sheria hii. Kila taasisi na mwajiri ni lazima watekeleze takwa hili la kisheria. Wito wangu kwa wafanyakazi kote nchini ni kwamba msigeuzi vyama hivyo kuwa vyanzo vya migogoro au migomo sehemu za kazi.

 

         Sambamba na hilo, napenda kuhimiza Wizara na taasisi mbalimbali kuhakikisha zinaunda Mabaraza ya Wafanyakazi kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6 ya Mwaka 2004. Nimeambiwa, mpaka sasa, yameundwa mabaraza ya wafanyakazi 487. Bado 28, yakiwemo 14 katika halmashauri na 14 mengine katika taasisi nyingine za umma.Nazihimiza taasisi ambazo hazijaunda mabaraza kufanya hivyo mara moja na kuhakikisha yanafanya kazi.

 

         Kuhusu suala la Mikataba ya Ajira kwa Wafanyakazi. Hili nalo sio suala la hiari. Kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya Mwaka 2004, waajiri wote wanapaswa kutoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wao. Kinyume chake ni kosa kisheria. Hivyo basi, namwagiza Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana kusimamia ipasavyo suala hili, hususan kwa kuimarisha ukaguzi na usimamizi . Aidha, Vyama vya Wafanyakazi navyo vinapaswa kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa kuwafichua waajiri wasiotoa mikataba ya ajira ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

        

         Kuhusiana na suala la Utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa, napenda kwanza kulishukuru Shirika la Kazi Dunia (ILO) kwa misaada mbalimbali inayotoa kwa nchi yetu, hususan yenye lengo la kukuza ajira, kupanua wigo wa hifadhi ya jamii na kuimarisha utekelezaji wa viwango vya kazi kimataifa. Napenda kuahidi kuwa Serikali itaendelea kusaini, kuridhia na kutekeleza mikataba ya kimataifa kuhusu masuala ya kazi na ajira yenye maslahi kwa wafanyakazi na Taifa kwa ujumla.

 

Na katika hili, napenda kuarifu kuwa katika Mkutano wa Bunge unaoendelea, Serikali imewasilisha Azimio la kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kazi za Ubaharia wa Mwaka 2006 (Marine Labour Convention) na Mkataba wa Kimataifa wa Vitambulisho Na. 185 wa Mwaka 2003 (Seafarer’s Identity Documents Convention). Kuridhiwa kwa Mikataba hii kutaongeza fursa za ajira kwa mabahari wa Tanzania na nchi yetu itanufaika na fursa za mafunzo na ajira.

 

Mheshimiwa Rais wa TUCTA;

Ndugu Viongozi wa TUCTA;

 Ndugu Wafanyakazi wenzangu;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

         Mbali na hatua za kushughulikia baadhi ya hoja ambazo zimetajwa kwenye Risala ya Katibu Mkuu wa TUCTA, Serikali pia inaendelea kuchukua hatua nyingine zenye lengo la kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya wafanyakazi nchini. Baadhi ya hatua hizo ni kama ifuatavyo:

 

         Kwanza kabisa, tumeendelea kuhimiza ujenzi wa Viwanda. Kama mnavyofahamu, kukua kwa sekta ya viwanda nchini kutaleta matokeo chanya kwa Watanzania wote, wakiwemo wafanyakazi. Hii ni kwa sababu viwanda vitaongeza mapato kwa Serikali na kuiwezesha kuboresha maslahi ya watumishi nchini. Lakini sio hivyo tu. Viwanda pia vitaongeza idadi ya wanachama kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Idadi ya wanachama ikiongezeka, Mifuko itaboresha mafao ya wanachama pindi wanapostaafu.

 

Nafurahi wito wa kujenga viwanda umepokewa vizuri. Viwanda vingi hivi sasa vinajengwa katika maeneo mbalimbali nchini. Hata Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF, PPF, PSPF na GEPF nayo imejitokeza kuwekeza kwenye sekta ya viwanda. Miradi ya viwanda yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 156 inatarajiwa kutekelezwa na mifuko hiyo. Viwanda hivyo ni vya Sukari (Mkulazi –Morogoro), Viatu (Moshi) na Viwatilifu vya kuulia vimelea vya malaria (Kibaha), ambavyo vitaajiri Wafanyakazi wapatao 310,000. Tunaendelea kuwahimiza wafanyabiashara wengine kuwekeza kwenye sekta ya viwanda, ikiwemo katika Mkoa huu wa Kilimanjaro, ambao Mheshimiwa Mkuu wenu wa Mkoa ameeleza kuwa zamani ulikuwa na viwanda vingi, lakini hivi sasa vimekufa.

 

         Mbali na kujenga viwanda, Serikali inachukua hatua nyingine mbalimbali zenye lengo la kuboresha maslahi ya wafanyakazi nchini. Hatua hizo ni pamoja na kuwaondoa watumishi hewa. Mpaka sasa tumeshawabaini watumishi hewa wapatao 19,706 ambao, kama wangekuwa hawajaondolewa, wangeigharimu Serikali kiasi cha shilingi bilioni 19.848 kwa mwezi, sawa na shilingi bilioni 238.17 kwa mwaka. Fedha hizi zingeweza kutumika kuboresha maslahi na mazingira ya kazi ya watumishi waliopo kazini au kufanya shughuli nyingine ambazo zingewanufaisha wafanyakazi. Ni kwa sababu hii, Serikali ililazimika kusitisha kwa muda zoezi la kuajiri na kupandisha vyeo watumishi. Kwa sasa, zoezi hili limefikia hatua nzuri, takriban asilimia 98.

 

         Sambamba na kuhakiki watumishi hewa, tulianzisha zoezi la uhakiki wa vyeti vya watumishi. Nchi yetu inaruhusu kila mtu kuajiriwa kulingana na elimu yake. Lakini wapo ambao wamekuwa wakitafuta vyeti vya kughushi ili kupata nafasi ambazo hawastahili. Wiki iliyopita nimepokea Taarifa kuhusu Ukaguzi wa Vyeti vya Wafanyakazi. Katika Ukaguzi huo, tumebaini kwamba, kati ya watumishi 400,035 wa Serikali za Mitaa, mashirika ya umma na taasisi za Serikali ambao wamehakikiwa, watumishi 9,932 wana vyeti vya kughushi; wakati watumishi 1,538 wana vyeti vyenye utata, kwa maana kwamba vyeti vyao vinatumiwa na zaidi ya mtu mmoja. Aidha, watumishi 11,596 waliwasilisha vyeti vya taaluma bila ya vyeti vya elimu. Watumishi wote wenye vyeti vya kughushi tumewapa hadi tarehe 15 Mei, 2017 kuwa wamejiondoa kazini. Kinyume na hapo, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

 

Ndugu Viongozi wa TUCTA na Ndugu Wafanyakazi wenzangu;

         Uwepo wa vyeti vya kughushi umesababisha matatizo mengi hapa nchini. Umepunguza tija katika utendaji wa kazi, umewakosesa watu wenye sifa ajira, vyeo na stahili mbambali, n.k. Na jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba, wengi wenye vyeti feki ni watoto wa viongozi na watu wenye uwezo. Mtoto wa maskini hawezi kupata fedha ya kununua cheti feki. Anajihangaikia mwenyewe.

 

         Baada ya kufikia hatua nzuri katika mazoezi haya ya uhakiki, Serikali sasa imepanga kuanza kuajiri tena. Kwenye Mwaka ujao wa fedha, tunatarajia kuajiri watumishi wapya wapatao 52,000 wa kada mbalimbali na pia tutaanza kuwapandisha tena madaraja watumishi. Aidha, katika mwaka ujao wa fedha, Serikali itatoa nyongeza ya kawaida ya mshahara kwa watumishi (annual increment). Lakini niseme tu kwamba uamuzi huu wa kuanza tena kuajiri, kupandisha madaraja na kutoa nyongeza ya mshahara, haumaanishi kuwa tumefikia mwisho. Bado tutaendelea na uhakiki wa watumishi hewa na vyeti. Zaidi ya hapo, tutaanza ukaguzi wa watumishi ambao wamebadilisha umri wao wa kustaafu.

 

Ndugu Viongozi wa TUCTA na Ndugu Wafanyakazi wenzangu;

         Suala jingine ambalo tunalishughulikia ni ulipaji wa madeni ya watumishi. Mathalani, tangu tumeingia madarakani mwezi Novemba 2015, tumelipa madeni ya walimu ya kimshahara yenye thamani ya shilingi bilioni 14.23 na pia tumelipa madeni ya watumishi yasiyo ya kimshahara yenye thamani shilingi bilioni 42.4. Tutaendelea kulipa madeni mengine kadri tutakavyokuwa tumejiridhisha kuwa hakuna udanganyifu. Hivyo, nawasihi sana wafanyakazi, mtuvumilie.

 

Kama mnavyofahamu, kumekuwa na tabia ya kutengeneza madeni ya uongo (madeni hewa). Mathalan, kuna baadhi ya viongozi wanashirikiana na watumishi kutengeneza uhamisho na kisha kugawana fedha hizo za uhamisho.  Wakati mwingine uhamisho umekuwa ukitolewa kwa sababu ya ugomvi binafsi kati ya kiongozi na mtumishi. Kwa sababu hiyo, naagiza, kuanzia sasa, ni marufuku kumwamisha mtumishi kabla ya kumlipa fedha zake za uhamisho.

        

Mbali na kulipa madeni ya watumishi, tumeweza kulipa madeni kwa ajili ya kutekeleza miradi mbali ya miundombinu ya barabara, umeme, maji na reli kiasi cha shilingi trilioni 3.68. Kati ya fedha hizo shilingi trilioni 1.1697 lilikuwa ni deni la wakandarasi wa barabara. Sambamba na hilo, tumetoa kiasi cha shilingi bilioni 80 kwa ajili ya kuwalipa wazabuni na watoa huduma mbalimbali, wakiwemo wanaotoa huduma katika shule na magereza yetu.

 

         Kama mnavyofahamu, madeni haya ya wakandarasi na wazabuni ilikuwa ni mzigo mkubwa kwa Serikali. Hivyo, baada ya kufanikiwa kupunguza mzigo huu, Serikali itaweza kuelekeza fedha kwenye shughuli nyingine, ikiwemo kuboresha mazingira na maslahi ya wafanyakazi. Lakini niseme tu kwamba, ingawa tumepunguza madeni, Serikali bado inadaiwa. Hivyo, hatutaweza kuelekeza fedha zote katika kuboresha maslahi ya wafanyakazi. Tutaendelea kulipa madeni na kuwekeza fedha tunazozipata kwenye shughuli nyingine za maendeleo, ambazo pia zitawanufaisha wafanyakazi. Mathalan, hivi sasa tunajenga reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa na tumenunua ndege sita. Mambo haya yote yatawanufaisha wafanyakazi na Watanzania kwa ujumla.

 

Ndugu Viongozi wa TUCTAna Ndugu Wafanyakazi wenzangu,

         Siwezi kuhitimisha hotuba bila ya kugusia masuala mengine machache ambayo baadhi yamegusiwa kwenye Risala ya Katibu Mkuu wa TUCTA. Kwanza kabisa ni kuhusu kaulimbiu ya Mei Mosi mwaka huu, ambayo inasema “Uchumi wa Viwanda Uzingatie Kulinda Haki, Maslahi na Heshima ya Wafanyakazi”. Hii ni kauli mbiu nzuri na imenipa moyo kuwa wafanyakazi mnatambua azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda. Nawahakikishia kwamba ujenzi wa viwanda utazingatia haki, maslahi na heshima ya kazi nchini. Lakini niwe muwazi tu kuwa, hatutamvumilia mfanyakazi mzembe na atakayetaka kutukwamisha katika kufikia azma yetu ya kujenga uchumi wa viwanda. Nimefarijika kusikia kwenye Risala yenu kuwa nanyi matuunga mkono. Risala yenu imeeleza kuwa TUCTA, nanukuu “…haitatetea wafanyakazi wavivu, wazembe, wabadhirifu, wala rushwa, wenye majungu, walevi wa kupindukia na wasiofuata sheria za kazi na za nchi…”, mwisho wa kunukuu. Nawashukuru sana kwa kutuunga mkono.

 

         Nimefurahi pia katika Risala ya TUCTA mmehimiza suala la amani nchini. Hili ni suala muhimu sana. Amani ndio msingi mkuu wa maendeleo. Bila ya amani, hakuna maendeleo. Nashukuru kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na biashara ya madawa ya kulevya. Ahsanteni sana.

        

Mmezungumzia pia kuhusu suala la Ugumu wa Maisha na Mfumko wa Bei ya Bidhaa Muhimu. Serikali imepokea suala hilo na tutalifanyia kazi. Lakini niseme tu kwamba Serikali imejitahidi sana kudhibiti mfumko wa bei nchini. Mathalan, mwezi Januari mwaka 2016, mfumko wa bei ulikuwa asilimia 7. Lakini kuanzia mwezi Machi tuliweza kuushusha hadi kufikia asilimia 4 na kiwango hicho kilidumu hadi mwezi Novemba 2016, ambapo mfumko wa bei ulianza kupanda tena na sasa umefikia asilimia 6.4, kutokana na kuchelewa kwa mvua kwenye baadhi ya maeneo ya Nchi yetu. Lakini sasa mvua zinanyesha katika maeneo mengi ya nchi yetu na hivyo nina uhakika mfumko wa bei utashuka.

        

Jambo jingine ambalo ningependa kuzungumzia ni suala la Makato ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Napenda niarifu kuwa kuwa tangu utaratibu wa kutoa mikopo ya elimu ya juu uanze mwaka 1994/95, Serikali imeshatoa jumla ya shilingi trilioni 2.9.  Mikopo ambayo imeiva hivi sasa ina thamani ya shilingi trilioni 1.4 na ambayo inapaswa kuwa imerejeshwa ni shilingi bilioni 427. Lakini mpaka sasa, ni shilingi bilioni 181.4 tu ndizo zimerejeshwa.  Hii maana yake ni kwamba kuna wanufaika wengi wa mikopo ambao hawataki kuirejesha. Ni kwa sababu hiyo, Serikali ilifikia uamuzi wa kuongeza makato kutoka asilimia 8 hadi asilimia 15 ili kuwezesha mikopo hiyo kurejeshwa haraka na kuwanufaisha wengine. Uamuzi huu unawalenga watu wote walionufaika na mikopo ya elimu ya juu. Hivyo, niwaombe TUCTA na Vyama vya Wafanyakazi kuwahimiza wanachama wenu kurejesha mikopo hiyo.

 

Ndugu Rais wa TUCTA;

 Ndugu Wafanyakazi wenzangu;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

         Nimeeleza mengi. Naomba niishie hapa. Lakini kabla sijahitimisha, napenda niwashukuru tena kwa kunialika kwenye shughuli hii. Nawaahidi wafanyakazi wote nchi kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira yenu ya kufanyia pamoja na maslahi yenu, kadri uwezo wa kufanya hivyo utakavyokuwa ukiongezeka.

 

Leo nimewaahidi kuwa tutaajiri watumishi wapya, tutaanza tena kupandisha vyeo na tutatoa nyongeza ya kawaida ya mshahara kwa watumishi katika mwaka ujao. Nimeagiza pia kuanzia sasa ni marufuku kwa mtumishi kuhamishwa kabla ya kulipwa fedha zake. Haya yote, tutayasimamia na kuyatekeleza ipasavyo.

 

Mungu Tubariki Wafanyakazi wa Tanzania!

Mungu Ibariki Tanzania!

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”