Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA SHEREHE YA UWEKAJI WA JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA INTERCHANGE YA UBUNGO TAREHE 20 MACHI, 2017

Thursday 20th April 2017

Mheshimiwa Dkt. Jim Yong Kim, Rais wa Benki ya Dunia;

 

Mheshimiwa Profesa Makame M. Mbarawa (Mb),

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano;

 

Waheshimiwa Mawaziri mliopo;

 

Mheshimiwa Balozi Mhandisi John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi;

 

Waheshimiwa Makatibu Wakuu mliopo;

 

Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;

 

Mheshimiwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam;

 

Mheshimiwa Prof. Norman Adamson Sigalla, Mwenyekiti

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu;

 

Waheshimiwa Wabunge na Madiwani wote mliopo;

 

Mheshimiwa Mama Bella Bird, Mwakilishi Mkazi wa Benki

ya Dunia Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia;

 

Watendaji Wakuu wa TANROADS;

Viongozi wa Serikali, Vyama vya Siasa na Dini mliopo;

Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana:

 

Kwanza kabisa, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha hapa tukiwa wazima. Aidha, napenda kutoa shukrani nyingi sana kwa Mheshimiwa Dkt. Jim Yong Kim, Rais wa Benki ya Dunia kwa kuja kutembelea. Kama inavyofahamika, Benki ya Dunia ni taasisi muhimu duniani; hivyo, kutembelewa na kiongozi wake ni jambo la heshima kubwa kwa nchi yetu. Tunamshukuru sana Dkt. Kim na tumefurahi kujumuika naye katika hafla hii ya kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Barabara za Juu (interchange) hapa Ubungo. Ujio wake hapa nchini ni ishara tosha kuwa anaipenda nchi yetu; na kwamba yeye ni rafiki wa kweli wa Watanzania.

 

Sisi Waswahili tuna usemi wetu usemao: “Mwenyeji njoo, mgeni apone”. Napenda kutumia fursa hii kuwaarifu Watanzania wenzangu kuwa ziara ya Mheshimiwa Dkt. Kim hapa nchini imekuwa ya mafanikio makubwa kwa nchi yetu. Imeleta neema kwa nchi yetu. Wakati wa mazugumzo yetu leo asubuhi nimemweleza mipango yetu mbalimbali na yeye amekubali kushirikiana nasi katika kuitekeleza. Tunamshukuru sana.

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Ni jambo lililodhahiri kuwa moja ya kero kubwa kwenye Jiji letu la Dar es Salaam, lenye wakazi wapatao milioni tano, ni suala la msongamano wa magari barabarani. Kwa kutambua hilo, mtakumbuka wakati wa kampeni, Chama changu kiliahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza jitihada zilizoanzishwa na Serikali zilizotangulia katika kushughulikia kero hiyo. Nafurahi utekelezaji wa ahadi hiyo, unaendelea vizuri. Tayari mambo mengi yamefanyika. Mara tu baada ya kuingia madarakani tulijenga barabara ya kilometa 4.3 kutoka Morocco hadi Mwenge, kwa kutumia fedha zilizopangwa kugharamia Sherehe za Uhuru. Aidha, mwaka jana mwezi Aprili  tuliweka Jiwe la Msingi la Barabara ya Juu (flyover) pale TAZARA na pia kuzindua Daraja la Nyerere (maarufu kama Daraja la Kigamboni). Aidha, barabara ya Dar es Salaam, Bagamoyo hadi Msata nayo imekamilika na hivyo imepunguza msongamano katika barabara ya Dar es Salaam-Chalinze. Hakuna shaka, uamuzi wetu wa kuhamia Dodoma nao umesaidia kupunguza foleni hapa Dar es Salaam.

 

Kama hiyo haitoshi, tarehe 25 Januari mwaka huu, tulifanya uzinduzi wa Mradi wa Usafiri wa Mwendokasi Awamu ya Kwanza. Mradi huo umehusisha ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 20.9 kutoka Kivukoni kwenda Kimara, Morocco na Gerezani. Tayari tumeanza kuona manufaa ya mradi huo.  Hivi sasa watu wanatumia wastani wa dakika 45 kutoka Kivukoni hadi Kimara, wakati awali, walikuwa wakitumia masaa mawili hadi matatu.

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Licha ya mafanikio yaliyopatikana katika Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Mwendokasi, mtakubaliana nami kuwa mradi huo unakabiliwa na tatizo kubwa hapa Ubungo. Kama mnavyofahamu, hapa Ubungo ndio lango kuu la usafiri wa barabara kwa nchi yetu. Magari mengi ya kwenda na kutoka mikoani pamoja na nchi jirani hupita hapa na hivyo kusababisha msongamano mkubwa wa magari katika eneo hili. Hata magari ya mwendokasi nayo yakifika hapa yanakwama.

 

Ni kutokana na kero hiyo, mtakumbuka kuwa siku ya uzinduzi wa usafiri wa mwendokasi, tukiwa pamoja na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika, Dkt. Mukhtar Diop, nilihimiza ukamilishaji wa majadiliano kuhusu ujenzi wa barabara za juu (interchange) hapa Ubungo.  Nafurahi, baada ya kama miezi miwili tu kupita, leo tupo hapa kusaini Mkataba wa Mkopo na kuweka Jiwe la Msingi la mradi huo. Nimefarijika sana na nawashukuru wote waliowezesha mradi huu kuanza kutekelezwa.

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Mradi huu wa interchange hapa Ubungo ni mkubwa na wa aina yake katika nchi yetu.  Utahusisha ujenzi wa barabara za juu za ghorofa tatu; na utakapokamilika, unatarajiwa kuondoa kabisa kero ya msongamano wa magari katika eneo hili.  Magari kutoka njia zote nne yatapita hapa bila kusimama na hivyo kurahisisha sio tu huduma ya usafiri wa mwendokasi bali kwa watumiaji wote wa barabara katika eneo hili. Sambamba na hilo, mradi huu utaboresha mandhari ya Jiji letu la Dar es Salaam, ambalo ni miongoni mwa Majiji yanayokua kwa kasi Barani Afrika.

 

Kwa sababu hiyo, napenda nitumie fursa hii, kwa niaba ya Watanzania wote, kuishukuru sana Benki ya Dunia kwa kutupatia mkopo wa kutekeleza mradi huu. Aidha, namshukuru tena Dkt. Kim pamoja na Mwakilishi wa Benki ya Dunia hapa nchini Mama Bird, kwa kubali kushiriki kwenye hafla hii. Kama alivyosema Mheshimiwa waziri, mradi huu utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 188.71. Kati ya fedha hizo, Benki ya Dunia itatoa takriban shilingi bilioni 186.725 kwa ajili ya usanifu, usimamizi na ujenzi wa mradi.  Serikali imetoa shilingi bilioni 1.985 kwa ajili ya fidia kwa wananchi wanaostahili kulipwa kwa mujibu wa sheria.

 

Lakini niseme tu kwamba huu sio mradi wa kwanza kufadhiliwa na Benki ya Dunia hapa nchini. Wamefadhili miradi mingi. Hivi sasa Benki ya Dunia inafadhili jumla miradi 28 hapa nchini yenye thamani ya takriban Dola za Marekani bilioni 4.2.  Baadhi ya miradi hiyo ni mradi wa maboresho ya usafiri wa reli; mradi wa maboresho ya mahakama;  mradi wa kupeleka umeme vijijini;  mradi wa maboresho ya Vyuo Vikuu vya Sokoine na Nelson Mandela;  mradi wa TASAF;  na pia mradi wa maboresho wa elimu ya msingi.

 

Mbali na miradi hiyo, muda mfupi tu ujao tutasaini mikataba ya kupata mkopo kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kutekeleza miradi mingine mipya mitatu. Miradi hiyo ni : 

(i)           Mradi wa Ujenzi wa Miundombinu ya Usafiri katika Jiji la Dar es Salaam (Dar es Salaam Urban Transport Project). Mradi huu, ambao thamani yake ni Dola za Marekani milioni 425, utahusisha ujenzi wa Interchange hii hapa Ubungo pamoja na miundombinu ya usafiri wa mwendokasi kwa Awamu ya Tatu na Nne;

(ii)         Mradi wa Usambazaji Maji safi pamoja na Utunzaji Mazingira na ukusanyaji wa maji taka wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 225. Tunataka kumaliza kabisa suala la maji hapa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla; na

(iii)       Mradi wa Kuboresha huduma katika miji ya Arusha, Dodoma, Kigoma, Mbeya, Mwanza na Mtwara wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 130.

 

Hii inafanya jumla ya mkopo tutakaopata leo kuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 780, sawa na takriban shilingi trilioni 1.74. Lakini kuna miradi mingine ambayo ipo njiani kuanza kutekelezwa yenye thamani ya takriban Dola za Marekani bilioni 1.284 ambayo ni sawa na shilingi trilioni 2.79. Miradi hiyo ni pamoja na upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam (USD milioni 345); mkopo kwa TANESCO (USD milioni 200); upanuzi wa mradi wa gesi (USD milioni 100); kilimo (USD milioni 100); elimu (USD milioni 224); na afya (USD milioni 200) na mkopo kwa Zanzibar (USD milioni 35). Mikopo hii inadhihirisha sio tu kuwa Benki ya Dunia ni washirika wetu wakubwa wa maendeleo, bali pia nchi yetu inakopesheka. Ndiyo, tunakopesheka. Tungekuwa hatukopesheki, Benki ya Dunia isingetupatia kiasi hiki kikubwa cha fedha. Napenda nimhakikishie Rais wa Benki ya Dunia kuwa tutalipa deni letu, hasa kwa kuzingatia kuwa masharti yao ni nafuu.

Wageni Waalikwa,

Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;

Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kupunguza kama sio kumaliza kabisa kero ya foleni za magari hapa Dar es Salaam. Mbali na ujenzi miundombinu ya usafiri wa mwendokasi, tumepanga kutekeleza miradi mingine ya miundombinu ya usafiri. Baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi wa Daraja la kupita juu ya bahari kutoka Aga Khan hadi Coco Beach lenye urefu wa kilometa 7 kwa mkopo kutoka Korea Kusini; ujenzi wa barabara za njia sita za kutoka Ubungo hadi Chalinze; na ujenzi wa barabara za juu kwenye maeneo ya Mwenge, Morocco, Magomeni na Tabata. Aidha, tupo kwenye maandalizi ya ujenzi wa babaraba za lami za mzunguko (Dar es Salaam Outer Ring Road) zenye urefu wa kilometa 34. Na katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17, Serikali imetenga fedha za ndani Shilingi billioni 38 kwa ajili ya kuboresha barabara za Jiji hili.

 

Sambamba na ujenzi wa miundombinu ya barabara, tunao mpango kabambe wa kuboresha huduma za usafiri wa reli katika Jiji la Dar es Salaam.  Aidha, ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge) nao unatarajiwa kupunguza tatizo la msongamano wa magari hapa Dar es Salaam. Hii ni kwa sababu mradi huo utahusisha pia ujenzi wa Kituo Kikubwa cha kupokea Mizigo pale Ruvu. Kituo hicho kikikamilika, magari ya mizigo hayataruhusiwa tena kuja Dar es Salaam kufuata mizigo Bandarini. Hivyo basi, tuna matumaini makubwa kuwa, kutokana na ujenzi wa miundombinu unaoendelea, muda mfupi ujao, suala la msongamano barabarani litakuwa historia hapa Dar es Salaam.

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana ;

Kabla sijahitimisha hotuba yangu, naomba nieleze masuala matatu ya mwisho. Jambo la kwanza ni kuhusu usimamizi wa mradi. Napenda kutoa wito kwa Wasimamizi wa Mradi huu kuhakikisha wanamsimamia ipasavyo Mkandarasi ili mradi huu ukamilike kwa viwango vinavyohitajika na ikiwezekana kabla ya wakati uliopangwa. Fedha zipo. Hivyo, hakuna sababu mradi huu kuchukua muda mrefu kutekelezwa. Watanzania wanausubiri kwa hamu mradi huu. Sambamba na hilo, nawasihi watu watakaopata kazi kwenye mradi huu kuwa waaminifu na wazalendo. Msiibe vifaa wala kuanzisha migomo isiyokuwa na sababu.

 

Jambo la pili, mradi huu unajengwa kwa gharama kubwa. Fedha zitakazotumika ni za mkopo na hivyo Serikali italazimika kuzilipa. Hivyo basi, niwaombe Watanzania wenzangu tuendelee kulipa kodi. Kodi ndiyo itakayowezesha Serikali kupata fedha sio tu kwa ajili ya kurejesha mkopo wa mradi huu, bali pia kutekeleza miradi mingine mbalimbali ya maendeleo.  

 

Suala la tatu na la mwisho ambalo napenda kuwaeleza Watanzania wenzangu ni kwamba, tujitahidi kuelekeza nguvu zetu kwenye masuala ya msingi yenye maslahi kwa nchi yetu. Nchi yetu inahitaji kuondokana na umasikini. Inahitaji kuwa na viwanda. Na sote hapa tunahitaji maendeleo. Haya ndiyo mambo yanapaswa yatuchukulie muda wetu mwingi kuyajadili. Tusipoteze muda kujadili mambo yasiyo na msingi, ambayo hayatupi majibu ya changamoto zinazotukabili.

 

Nafahamu mnao uhuru wa kujadili mnachopenda lakini huo ndio ushauri wangu kwenu. Nchi yetu inahitaji maendeleo. Tunapaswa sote tushirikiane katika kuijenga nchi yetu. Hii ndio sababu nimefurahi sana leo hapa tunao viongozi wa vyama mbalimbali. Hivi ndivyo inavyotakiwa. Maendeleo hayana Chama. Sote tukishirikiana nchi yetu itapiga hatua kimaendeleo na kuwa mfano wa kuigwa Barani Afrika.

 

Mheshimiwa Dkt. Kim;

Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:

 Napenda kuhitimisha kwa kumshukuru tena Rais wa Benki ya Dunia kwa kuja kuungana nasi katika hafla hii na pia kwa misaada mbalimbali ambayo Benki ya Dunia imekuwa ikitoa kwa nchi yetu. Napenda nimhakikishie kuwa fedha zote wanazozitoa zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Hakuna fedha itakayopotea.

 

Mwisho lakini sio kwa umuhimu napenda kuishukuru Wizara ya Ujenzi pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu mbalimbali iliyowezesha kuanza utekelezaji wa mradi huu. Ahsanteni sana.

 

Baada ya kusema hayo, sasa niko tayari kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Barabara za Juu (interchange) hapa Ubungo.

 

Mungu Wabariki Wana-Dar es Salaam!

Mungu Ibariki Tanzania!

Mungu bariki mahusiano kati ya Tanzania na Benki ya Dunia!

 

“Asanteni Sana kwa Kunisikiliza”.