Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHE. DKT, JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA DHIFA YA KITAIFA ALIYOIANDAA KWA HESHIMA YA MHESHIMIWA JACOB ZUMA, RAIS WA AFRIKA KUSINI IKULU, DAR ES SALAAM, TAREHE 11 MEI, 2017

Thursday 11th May 2017

Mheshimiwa Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini

na Mama Sizakele Zuma;

 

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais

wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein, Rais wa Zanzibar

na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;

Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu

wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Bunge la Tanzania;

Mheshimiwa Prof. Ibrahim Juma, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania;

Waheshimiwa Marais Wastaafu mliopo;

Mheshimiwa Makamu wa Rais Mstaafu na Mawaziri Wakuu Wastaafu;

Waheshimiwa Mawaziri wa Afrika Kusini na Tanzania mliopo;

Waheshimiwa Mabalozi mliopo;

Waheshimiwa Viongozi wengine wa Serikali,

Vyama vya Siasa na Dini mliopo;

 

Wakuu wa Vyombo Vya Ulinzi na Usalama;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana:

         Awali ya yote, kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kwa mara nyingine tena nikushukuru kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais Zuma kwa kukubali mwaliko wetu wa kuja kututembelea. Natambua vizuri kwamba hii si mara yako ya kwanza kutembelea nchi yetu. Umeshatembelea mara kadhaa. Lakini napenda nikuthibitishie kuwa mimi pamoja na Watanzania wenzangu tumefarijika sana kwa ujio wako. Tunayo matumaini makubwa kuwa ziara yako hii, kama nyingine zilizotangulia, itakuza zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya mataifa yetu mawili.

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

         Tupo hapa kwa ajili ya Chakula tulichokiandaa kwa heshima ya wageni wetu, Mheshimiwa Rais Zuma na Mkewe Mama Sizakele Zuma pamoja na ujumbe wao. Na kama mnavyofahamu, katika tamaduni nyingi za Kiafrika, wakati wa chakula, sio wa kuzungumza. Lakini kwa leo naomba mnivumilie niseme japo mambo machache.

 

Kwanza kabisa, napenda niseme kuwa Tanzania na Afrika Kusini ni nchi marafiki na pia ni ndugu. Urafiki na udugu wetu una historia ndefu. Baadhi yenu mtakuwa mkikumbuka kuhusu vita vya mfecane na historia ya Kabila la Wangoni lililopo Kusini mwa Tanzania, ambalo asili yake ni Afrika Kusini. Lakini ukiachilia mbali historia hiyo ya Wangoni, wengi mnafahamu kuwa wakati wa utawala dhalimu na wa kibaguzi nchini Afrika Kusini, Tanzania ilishirikiana kwa karibu na wananchi wa Afrika Kusini, hususan kupitia Chama chao cha ANC.

Kufuatia makubaliano yaliyofikiwa mwaka 1962 kati ya viongozi wetu wawili, yaani Baba wa Taifa letu, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati Mzee Nelson Mandela, Tanzania ilitoa msaada kwa wapigania uhuru wa Afrika Kusini, ikiwemo kuwapatia mafunzo wapiganaji wake katika makambi yaliyopo Kongwa, Dakawa, Mazimbu, Mgawawo na kule Iringa.Kutokana na uhusiano huo wa kihistoria, haishangazi leo hii kuona kuwa Mataifa yetu mawili yana Nyimbo za Taifa zinazofanana; Bendera zetu zinashabihiana; lakini pia vyama vyetu tawala, yaani CCM na ANC vinashirikiana kwa karibu sana.

 

Na bila shaka, hii ndiyo sababu pia kuwa, tangu kurejea kwa utawala wa wengi nchini Afrika Kusini mwaka 1994, ushirikiano wetu kiuchumi nao umeimarika. Taifa la Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi 10, ambazo ni washirika wakuu wa Tanzania katika biashara na uwekezaji. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, biashara kati yetu ilifikia thamani ya shilingi za Tanzania trilioni 2.4 mwaka 2016, wakati uwekezaji wa Afrika Kusini hapa nchini hivi sasa una thamani ya Dola za Marekani milioni 803.15 na umetoa takriban ajira 20,916. Hii ni kudhihirisha kuwa uhusiano wetu ni mzuri; na unakua kila kukicha.

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Katika Ziara hii ya Mheshimiwa Zuma hapa nchini, tumeweza kufanya Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Marais ya Ushirikiano (Bi-National Commission - BNC). Katika Mkutano huo, tumejadiliana kwa kirefu kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali, ikiwemo biashara na uwekezaji; maendeleo ya viwanda, miundombinu; kilimo; afya; elimu; sayansi na teknolojia; ulinzi na usalama; nishati na madini; pamoja masuala ya maliasili na utalii. Na tumehimizana katika kusimamia utekelezaji wa makubaliano tuliyofikia. Aidha, tumekubaliana kuharakisha utekelezaji wa Mikataba yote iliyosainiwa na nchi zetu siku za nyuma, ambayo kwa sasa imefikia 16, ukiwemo mmoja tuliousaini leo.

 

Lakini mbali na kufanya Mkutano wa Tume yetu ya Ushirikiano, katika ziara hii, Mheshimiwa Rais Zuma ameambatana na wafanyabiashara wapatao 80. Kwa siku nzima ya leo, wafanyabiashara hao wamekutana na wenzao wa Tanzania. Na nimeambiwa kuwa Mkutano ulikuwa ni mzuri sana. Wamepashana habari kuhusu fursa za biashara na uwekezaji zilizopo katika nchi zetu; na pia wamebadilishana uzoefu na kupeana mbinu za kufanya biashara. Hivyo basi, nina uhakika, muda mfupi ujao, tutaona matunda yake. Namshukuru tena Mheshimiwa Rais Zuma kwa kufanya ziara, ambayo imekuza zaidi ushirikiano kati yetu.

 

Mheshimiwa Rais Zuma na Mama Sizakele Zuma;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

 Niliahidi kuzungumza kwa kifupi. Lakini siwezi kuhitimisha hotuba yangu bila ya kumpongeza Mheshimiwa Rais Zuma, Serikali na Wananchi wote wa Afrika Kusini kwa kuadhimisha Miaka 23 ya kumalizika kwa utawala wa kibaguzi hapo tarehe 27 Aprili, 2017. Hakuna shaka, katika kipindi hicho Afrika Kusini imepiga hatua kubwa, hususan katika kujenga haki, usawa na demokrasia. Afrika Kusini pia imetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Kanda yetu ya SADC, Bara letu la Afrika na Duniani kwa ujumla. Napenda kuahidi kuwa Tanzania chini ya uongozi wangu itaendelea kushirikiana na Afrika Kusini ili kudumisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wa kidugu na kihistoria kati yetu.

 

Baada ya kusema hayo, mabibi na mabwana, kwa heshima na taadhima, sasa naomba sote tusimame na kisha tunyanyue glasi zetu juu:

  • Kwa ajili ya afya njema ya Rais Jacob Zuma na Mama Zuma;
  • Kwa Ustawi wa Uhusiano wa Tanzania na Afrika Kusini; na
  • Kwa Maendeleo ya nchi zetu mbili na watu wake.

 

“Ahsanteni kwa kunisikiliza”.